Genesis 28:10-22

Ndoto Ya Yakobo Huko Betheli

10Yakobo akatoka Beer-Sheba kwenda Harani. 11Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake akajinyoosha akalala usingizi. 12 aAkaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake. 13Juu yake alisimama Bwana, akasema, “Mimi ni Bwana, Mungu wa baba yako Abrahamu na Mungu wa Isaki. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako. 14 bUzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako mataifa yote ya duniani yatabarikiwa. 15 cNiko pamoja nawe nami nitakulinda kila uendako na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”

16 dYakobo alipoamka kutoka usingizini, akawaza, “Hakika Bwana yuko mahali hapa, wala mimi sikujua.” 17 eKwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”

18Asubuhi yake na mapema, Yakobo akalichukua lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo na kumimina mafuta juu yake. 19 fMahali pale akapaita Betheli,
Betheli maana yake Nyumba ya Mungu.
ingawa mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.

20 hKisha Yakobo akaweka nadhiri, akisema, “Kama Mungu akiwa pamoja nami na kunilinda katika safari niendayo, akinipa chakula nile na nguo nivae 21 ina nirudi salama nyumbani kwa baba yangu, hapo ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu, 22 jnalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu na katika yote utakayonipa nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

Copyright information for SwhNEN